
Kutoka Vijiweni Kwenye Utajiri wa Akili: Mapinduzi ya Michezo ya Ubao Tanzania
Kwa miaka mingi, mchezo wa drafti nchini Tanzania umeonekana kama burudani ya watu waliokosa shughuli za kufanya. Licha ya faida lukuki zinazotokana na mchezo huu, bado hatujaupa thamani inayostahili wala kuutumia kwa maslahi ya kizazi kijacho. Mara nyingi, drafti huchezwa vijiweni, maeneo ya biashara, na sehemu zenye mikusanyiko ya watu, huku likivutia washiriki wa rika zote.
Tofauti na hapa kwetu, nchi za Ulaya na Asia hutumia michezo ya ubao (Board Games) kama zana ya kukuza uwezo wa kufikiri na kuendeleza vipaji vya watoto mashuleni. Michezo kama Chesi na Drafti imeratibiwa vyema kimashindano katika ngazi zote, jambo ambalo huongeza ushiriki wa jamii na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa wanamichezo hao.
Tanzania, na Afrika kwa ujumla, bado tunakabiliwa na upungufu wa mifumo thabiti ya kutambua na kukuza vipaji katika michezo hii. Hata hivyo, kutokana na kasi ya maendeleo ya kiteknolojia, tuna nafasi ya kipekee ya kubadili hali hii. **Tzdraft** ni jukwaa linalokuja na maono ya kuleta mapinduzi katika drafti, chesi, na bao la kete. Kupitia mifumo ya kidijitali ya Tzdraft, tutaweza kuratibu mashindano ya kitaifa, kuongeza ushiriki wa jamii, na kuunganisha michezo hii na vumbuzi za kiteknolojia kwa manufaa ya taifa.